top of page
Search

MIZIZI YA UKOLONI NDANI YA FIKRA ZA WATANZANIA

  • Writer: Humphrey Makussa
    Humphrey Makussa
  • May 26, 2017
  • 7 min read

Paukwa……Pakawa, Haya ni maneno ambayo hapo zamani wazee wetu waliyatumia pale msimuliaji wa hadithi ambaye kifasihi anajulikana kama fanani alitumia neno paukwa kabla ya kuanza hadithi yake na msikilizaji huitikia pakawa anaitwa hadhira. Lengo la matumizi ya maneno haya ni kuandaa utulivu na utayari wa fanani na hadhira tayari kwa kuwasilisha na kupokea ujumbe wa hadithi husika.

Leo nimekumbuka simulizi za zamani ambazo kupitia babu zetu tuliburudika na kujifunza mambo mengi yahusuyo tamaduni zetu, utawala, shughuli za maendeleo na uzalishaji. Hivyo nimejikuta nikitafakari mambo mengi yanayotokea hivi sasa nikijaribu kuoanisha na simulizi za mambo yaliyotokea hapo zamani.

Paukwa…… ni matumaini yangu umeitikia pakawa. Historia ni somo linalotupa simulizi ya mambo yaliyopata kutokea siku za nyuma kwa lengo la kuonya, kuburudisha ama kuelimisha vizazi vipya juu ya mambo yaliyotokea hapo zamani. Sakata la mchanga wa dhahabu (Makinikia) limenifanya nimkumbuke mwalimu wangu wa Historia nilipokuwa sekondari na somo la uchumi wa kikoloni Afrika.

Mwalimu wangu alinifundisha kuwa uchumi wa kikoloni ulikuwa na lengo la kuhakikisha upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vyao ulaya na masoko ya mazao yatakayozalishwa, ndiyo maana miundombinu yote iliyowekezwa nchini ilikuwa na mlengo wa kurahisisha upatikanaji na usafirishaji wa malighafi na rasilimali zetu kutoka kwenye migodi na mashamba hadi mwambao wa pwani tayari kwa kusafirishwa ulaya.

Lakini pia machifu na watawala wa kiafrika waliingia mikataba ya kilaghai iliyopelekea kupoteza haki za waafrika kumiliki ardhi, migodi na mashamba. Mikataba ambayo watawala hao waliambulia zawadi kama vito vya thamani ndogo, vioo na shanga. Hivyo kutusababishia unyanyaswaji, ukandamizwaji na unyonjwaji uliopelekea umasikini wa waafrika na utajiri wa watu weupe. Nachelea kusema umasikini wetu ni zao la upofu wa fikra za machifu na watawala wetu.

Ripoti ya Prof. Abdulkarim H. Mruma mwenyekiti wa kamati teule ya rais Magufuli kuchunguza makontena 277 ya mchanga wa dhahabu yaliyoshikiliwa bandarini, imewafungua macho watanzania walio wengi juu ya unyonyaji na uporaji wa utajiri wa maliasili ya watanzania. Utajiri ambao kama ungetumika vizuri, nchi yetu ingekuwa na uwezo mkubwa wa kutumia pato lake la ndani kwa maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Kwa muda mrefu watanzania tumekuwa tukiibiwa kupitia kivuli cha uwekezaji, jambo la kusikitisha zaidi ni kuona viongozi wetu ambao rasilimali zetu zimetumika kuwaelimisha ili kuikomboa Tanzania katika dimbwi la umasikini na unyonyaji wa kikabaila, wamekuwa mstari wa mbele kushirikiana na makabaila hao kwa kuchimba mifereji ya kurahisisha unjonyaji wa rasilimali zetu.

Miaka ya 1998 Tanzania iliingia mikataba ya uchimbaji wa madini na kampuni ya kimataifa iliyojulikana kama African Barrick Gold plc hivi sasa Acacia Mining. Wawekezaji hawa walianza kazi za uchimbaji miaka ya 2000 kwa kununua mali za makampuni ya Bulyanhulu, Buzwagi na baadaye North Mara. Kutokana na mikataba waliyoingia kisheria, mwekezaji huyu aliruhusiwa kusafirisha nje mchanga wa dhahabu (Makinikia) kwaajili ya kufanya uchenjuaji (Smelting) kutenganisha madini ya dhahabu, shaba, fedha na madini mengine kama chuma.

Serikali ya awamu ya tatu chini ya Waziri mwenye dhamana wa Nishati na Madini Daniel Yona, iliingiza Tanzania kwenye mkataba wa kinyonyaji na usio wa kizalendo kwa taifa. Mkataba ambao kwa kipindi cha miaka 17 ya uchimbaji, kampuni ya Acacia inakadiriwa kusafirisha zaidi ya kontena 61,000 za mchanga wa dhahabu ambao kutokana na hesabu za utafiti wa kamati maalumu ya Mruma, ni sawa na tani za ujazo 3,264. Kwa tafsiri ya kawaida hii ni sawa na lori 466 zenye uzito wa tani saba zilizojaa dhahabu.

Hivyo, thamani halisi kwa makadilio ya chini ni zaidi ya shilingi trilioni 169 za kitanzania. Fedha ambazo kwa mlinganisho wa bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 ambayo ni trilioni 29.5 zingeweza kutumika kama bajeti ya taifa kwa miaka mingine sita. Huu ni unyonyaji wa rasilimali za watanzania, unyonyaji unaofanywa na wawekezaji wakitengenezewa mazingira na watawala tuliowaamini tukawapa dhamana ya uwakilishi wa watanzania walio wengi. Lakini watawala hao wametusaliti na kuweka mbele maslahi yao binafsi kwa kuingia mikataba inayotunyonya na kutugandamiza.

Tumekuwa na mifano hai kadha wa kadha inayoonesha matumizi mabaya ya madaraka na mali za uma. Ndani ya kipindi cha muda mfupi tuu achilia mbali nyanja nyingine, katika nyanja hii ya nishati na madini watanzania tumeshuhudia madudu mengi yaliyofanywa na watu tuliowapa dhamana ya kutuwakilisha katika ngazi mbalimbali za maamuzi hata kupelekea kuwajibishwa kwao.

Mwaka wa 2005 aliyekuwa raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa awamu ya tatu akishirikiana na waziri wa Nishati na Madini Mh. Daniel yona kinyume cha sharia walijimilikishia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira Mbeya (Kiwira Coal Mine) kupitia kampuni yao ya Tanpower Resources Company Limited. Ikumbukwe pia mwaka 1998 Mh. Daniel yona aliliingiza taifa katika mkataba wa kinyonyaji na African Barrick Gold plc hivi sasa Acacia Mining.

Miaka ya 2006/2008 Mh. Nazir Mustafa Karamagi aliwajibishwa baada ya kuliingiza taifa katika mkataba wa kusambaza megawatts 100 za umeme wa dharura katika kipindi cha ukame kwa dola za kimarekani milioni 172.5 ambayo kwa makadilio ya sasa ni zaidi ya shilingi za kitanzania bilioni 385. Lakini genereta la kuzalisha umeme huo lilichelewa kuingizwa nchini na lilikuwa bovu hivyo kulisababishia taifa hasara. Ibrahim Msabaha waziri wa zamani wa nishati na madini na Waziri mkuu wa wakati huo Edward Lowasa walilazimika kujiudhuru kutokana na kashfa hii.

Lakini pia, kipindi cha 2008/2012 Mh. Willium Ngeleja alilazimika kuachia madaraka kwa kashfa ya rushwa miongoni mwa viongozi waliopokea mgao wa fedha shilingi 306.6 bilioni zilizochotwa kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow baada ya kukili kupokea shilingi milioni 40.4 kutoka kwa mmiliki wa kampuni tanzu VIP Engeneering and Marketing James rugemalira.

Nafasi ya Uwaziri wa Nishati na Madini ilichukuliwa na Mh. Sospiter Muhongo katika kipindi cha 2012/2015, hata hivyo kabla ya kumalizika kwa kipindi cha awamu ya nne rais Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wake kutokana na sakata la Tegeta Escrow. Muda mfupi baada ya kuingia madarakani Rais Magufuli alimteua tena kua waziri wa Nishati na Madini hadi alipolazimishwa kujiudhuru tarehe 24 Mei 2017 kutokana na kahfa ya usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (Makinikia).

Hatuna budi kuamini kuwa uchumi wa kikoloni na fikra mgando za viongozi wetu tuliowapa dhamana ni sababu kubwa ya kuporwa kwa rasilimali zetu na mataifa yaliyoendelea. Hivyo kama tunataka kuendelea, hatuna budi kubadiri fikra mgando tulizojazwa na uchumi wa kikoloni kuwa mataifa yanayoendelea hatuwezi kujitegemea wala kuzalisha pasipo ngozi nyeupe. Hizi ni fikra potofu ambazo kama tutashindwa kuzikabili na kuwa wazalendo katika kupigania stahiki na maendeleo yetu binafsi kama taifa, kamwe hatutaweza toka katika dimbwi la unyonywaji chini ya kivuli cha wawekezaji.

Nchi hii inahitaji watu wenye maamuzi magumu katika kuleta mabadiliko, tunaitaji watu wenye uthubutu bila kuangalia tamaduni zilizozoeleka katika utendaji. Tunahitaji kuwa na taifa lenye watu wenye misimamo na uzalendo, watu walio tayari kupigania haki zao na kuwatia moyo wale wanao simamia haki, utawala bora, mabadiliko chanya na maendeleo ya taifa bila kuwakatisha tamaa.

Nitumie nafasi hii kumpongeza raisi wangu mteule Dr. John Joseph Pombe Magufuli jembe la watanzania. Hakika taifa limempata rais, kiongozi sahihi aliyekuwa akitarajiwa ili kuleta mabadiliko kwa faida ya watanzania walio wengi na si faida kwa tabaka la watawala na watu wachache wenye nguvu ya pesa. Watu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakijilimbikizia mali na kutumia vibaya nguvu ya pesa walizonazo kuwagandamiza na kuwanyanyasa walala hoi ambao ndiyo lulu ya uzalishaji katika taifa hili.

Kupitia ripoti ya kamati teule kuchunguza Kontena za makinikia, Rais Magufuli ameonesha nia ya dhati aliyonayo katika kulikomboa taifa kutoka katika mikono ya wanyang’anyi chini ya kivuli cha uwekezaji. Hii imefanya imani niliyokuwa nayo kwake katika kuleta mabadiliko ya taifa hili iongezeke mara dufu. Ni wazi kuwa kupitia ripoti hii rais ataongeza idadi ya maadui ambao kiuhalisia wamekuwa wakijifaidisha wao binafsi kwa rasilimali za watanzania, lakini bila kujali hilo raisi wetu ameendelea kusimamia haki na kuchukua maamuzi magumu kwa niaba ya watanzania wote.

Kutokana na uhuru wa habari na maendeleo ya tekinolojia, kwa maslahi binafsi ama itikadi za kidini na kisiasa baadhi ya watanzania na watu wenye heshima katika taifa hili wamekuwa mstari wa mbele kuanzisha mijadala yenye dhihaka ili kukatisha tamaa jitihada zinazofanywa na wazalendo wa nchi hii ambao hawakubaliani na kuongozwa kwa mazoea, viongozi ambao wamedhamiria kuleta mabadiliko kwa faida ya umma. Hili ni zao la mizizi ya ukoloni ndani ya fikra za watanzania.

Mwanasiasa na mwanasheria makini anayeaminika na kukubalika katika kutetea na kusimamia haki za watanzania, kwa mtazamo wake ameandika andiko kupitia mitandao ja kijamii linalomtuhumu rais kuzuia makontena ya mchanga akisema “Tuna JPM anayeamini kwamba ametumwa na Mungu kuinyoosha nchi hii na neno lake ndiyo sharia. Matokeo yake atagombana na mabwana wakubwa wa kifedha duniani ambao ndiyo wamiliki halisi wa rasilimali zetu”. Tundu Lissu hii hainiingii akilini, inaonesha fikra mgando tulizonazo zilizoathiriwa na uchumi wa kikoloni. Rasilimali za Tanzania ni mali ya watanzania na si mabwana wakubwa wa kifedha huko ulimenguni.

Kaka yangu Zitto Kabwe Mwanasiasa na Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini apingana na uamuzi wa kuzuia usafirishaji wa makontena ya makinikia. Alisema “amri ya rais kuhusu machanga wa dhahabu imeipotezea nchi Tshs 1.8 Trilion capital gains tax…. Niliwaeleza wanachama na wageni wengine katika mkutano wa ACT Wazalendo kuwa amri ya kiholela aliyoitoa rais john Magufuli kuzuia usafirishaji wa mchanga wa dhahabu imepelekea nchi yetu kupoteza USD 880m kama kodi ya ongezeko la mtaji kutokana na mauzo ya Acacia Mining”

Nachelea kupingana na Mh. Kabwe kwani kuacha biashara iendelee ni sawa na kuruhusu unyoywaji tunaofanyiwa uendelee, ni bora kupoteza kiasi cha mapato yatakayotokana na kodi sasa kuliko kupoteza kiwango kilichoibuliwa na kamati ya Prof. Mruma. Pia bila maamuzi magumu aliyochukua mh. Magufuli watanzania tungejua lini kama tunaibiwa kwa ukubwa huo. Hoja ya kujenga kwanza mitambo ya uchenjuaji haina mashiko sana kwani bado tunaweza kuzuia usafirishaji wa makinikia huku taratibu za ujenzi wa mitambo zikiendelea kwani madini hayaozi. Hoja hapa ni bora kupoteza mapato sasa ambayo wachache na wawekezaji ndiyo wanao faidi lakini hapo baadaye tukazalisha zaidi kwa faida ya watanzania.

Pamoja na ukweli kuwa wapo wengi waliodhihaki na kukejeli juhudi za mweshimiwa rais wakiwepo baadhi ya wanazuoni na wahadhiri wa vyuo vikuu, lakini wapo pia walioungana na watanzania walio wengi kumpongeza raisi katika hatua aliyochukua dhidi ya wanyonyaji. Niwapongeze Mh. David Kafulila, Dr. Kigwangala, Umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) na Comrade Mbilinyi Jr, hawa ni baadhi ya wengi wanaounga mkono juhudi za jembe la taifa Mh. Magu.

Kama nilivyoanza kwa kusema historia ni somo lililokuwa na lengo la kutukumbusha mambo yaliyotokea zamani kwa lengo la kutuelimisha na kutuonya, lakini chakusikitisha tumesoma na baada ya kumaliza masomo tumefunika madaftari na kusahau unyonywaji tuliofanyiwa na wakoloni na bado tunaendelea kuwakumbatia.

Nimalize kwa kusema kuwa umasikini wa Tanzania ni zao la upofu wa fikra uliojengwa na mizizi ya ukoloni kupitia kivuli cha uwekezaji. Hivyo hatuna budi kuzinduka, kukemea unyonyaji unaofanywa na mabwanyenye na tabaka la watu wachache waliojilimbikizia mali. Tukiwa na umoja kama taifa tutaishinda ukoloni mamboleo na kulinda rasilimali za taifa zinazoporwa kwa mgongo wa uwekezaji.


 
 
 

Join our mailing list

  • Black MySpace Icon
  • Google+ Social Icon
  • Facebook Social Icon
  • LinkedIn Social Icon
  • Instagram Social Icon
  • Twitter Social Icon
  • YouTube Social  Icon

© 2017 by PSM Productions. Proudly created by P-Skills with Wix.com

bottom of page